Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kukamatwa kwa Msanii wa Filamu Tanzania, Wema Sepetu kwa kukiuka masharti ya dhamana.
Uamuzi huo umetolewa na hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama hiyo, Maria Kasonde baada ya Mshitakiwa kushindwa kufika Mahakamani kusikiliza kesi inayomkabili.
Wema anakabiliwa na kosa moja la kusambaza picha zisizo na maadili kwenye mitandao ya kijamii analodaiwa kulitenda Mwishoni mwa mwaka 2018.
Wakili wa Wema Sepetu, Ruben Simwanza alisema kuwa, Mteja wake alikuwepo Mahakamani lakini aliugua ghafla na kulazimika kuondoka.
“Kama amekuja Mahakamani halafu akaondoka bila kutoa taarifa, Mahakama itajuaje kama alikuja? Alishindwa kutoa taarifa Mahakamani” Alihoji Hakimu Maria Kasonde.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Kasonde amehairisha kesi hiyo hadi Julai 4 Mwaka huu huku akitoa hati hiyo ya Wema kukamatwa.




