Msanii wa muziki wa Rap chini Tanzania, Ibrahim Mussa maarufu kama Roma au Roma Mkatoliki aliyeko nchini Marekani kwa sasa, ameeleza juu ya nia ya kuisaida jamii kupitia sanaa ikiwa yeye na msanii mwenzake Stamina, wao kama ‘ROSTAM’, wanafanya vizuri na wimbo wao ‘Kaka Tuchati’, wimbo ambao umezungumzia janga la Ugonjwa wa Corona kwa asilimia kubwa.
Akitoa maelezo juu ya nia yao hiyo kupitia Insta Live kwenye Ukurasa wake, Roma alieleza kuwa kwa nafasi yake akishirikiana na Stamina, wamekubaliana na kutambulisha ‘Challenge’ ya kuchangisha kiasi kidogo kidogo cha fedha kutoka kwa mashabiki wao na watu wote watakaoguswa na nia yao ya kupata fedha za kununua Mashine ya kusaidia uingizaji hewa kwa matibabu ‘Ventilator Machine’.
Challenge hiyo kutoka kwa Roma Na Stamina itakayoendeshwa kwa muda wa takribani wiki mbili iliyotambulishwa Mei 16 2020, itakwenda kwa jina la ‘Kaka Tuchati Ventilator Challenge’ ambapo Roma aliweka bayana kuwa wameanzisha hilo na wako tayari kushirikiana na mamlaka husika nchini Tanzania kufanikisha nia yao kama wasanii.
Hata hivyo katika mazungumzo ya Moja kwa moja muda mfupi baada ya kulitangaza hilo, Roma akizungumza na Mtangazaji kutoka kituo cha Matangazo cha BBC Idhaa ya kiswahili, Bi. Zuhura Yunus aliyeko London alionesha kuguswa na kupenezwa na wazo hilo la Roma na Stamina na pale pale alitoa ahadi ya kuchangia kiasi cha shilingi laki moja na nusu (150,000tsh) katika kuunga mkono juhudi hiyo.

Wimbo wa Roma na Stamina, ‘ROSTAM’, ‘Kaka Tuchati’.




